Beni, DR. Congo

Watu kumi na saba (17) wamejeruhiwa kwenye mripuko wa bomu uliotokea mjini Beni, nchini Demokrasia ya Congo.

Mripuko huo umetokea mwendo wa saa moja kasorobo wakati mlio wa bomu ulisikika eneo kubwa la mji wa Beni. Bomu hilo lilitegwa kwenye jengo la mtambo wa kusagia unga wa mahindi pamoja na mihogo kwenye soko ya Macampagne, Kata ya Kalinda mjini Beni, nchini Demokrasia ya Congo.

Walioshuhudia mkasa huo, akiwemo kijana anayefanya kazi ya kusaga unga kwenye jengo hilo, wanasema, kuna mwanamume mmoja aliyeweka mfuko wake wa plastiki kwenye jengo hilo na kuondoka.

Kulingana na mashuhuda ni baada ya dakika tano ndio bomu liliripuka na kuwajeruhi watu kadhaa.

Majeruhi walipokuwa wanapelekwa kwenye vituo vya afya kwa matibabu, maofisa wa jeshi la polisi ya Congo pamoja na washirika wao wa polisi ya Umoja wa mataifa, waliwasili katika eneo la tukio, na kuanzisha uchunguzi.

Shambulio la tatu la bomu

Mji wa Beni ukiwa kila mara unashambuliwa kwa mabomu ya kutengenezwa nyumbani, na shambulio la jana Jumatano likiwa linatokea siku zaidi ya kumi baada ya lile la Kasindi kwenye kanisa la madhehebu ya CEPAC, msemaji wa jeshi la polisi mjini Beni amewaomba wakaazi kuwa waangalifu, huku akiwasihi kutokaribia vifurushi ambavyo hawajui vina nini ndani.

Mashambulio ya kila uchao yanayofanywa na kundi la kigaidi kutoka Uganda ADF katika maeneo mbalimbali ya Beni, yanatokana na mkung’uto wanaoupata kutoka kwa majeshi ya muungano yaani jeshi la Congo FARDC na lile la Uganda, UPDF, katika ngome zao mbalimbali, katika wilaya za Beni na Irumu.

Msemaji wa jeshi la Congo FARDC wa sekta ya operesheni Sokola1 grand nord, kapteni Anthony Mualushayi aliiambia DW, kwamba ADF wakiwa hawana uwezo wa kupambana na jeshi la Kongo, wamekuwa wakilipiza kisasi kwa kuwashambulia wananchi, na kwamba, hatua madhubuti zimechukuliwa na vyombo vya dola, ili kuhakikisha kwamba mashambulio mengine hayatokei.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wakaazi wa mji na wilaya ya Beni, kuwa wanawataarifu wanajeshi, wanapoona watu wasiojulikana katika maeneo yao, na hasa kuanzisha operesheni chunguza jirani.

Majeruhi wa shambulio la jana, wanatibiwa, baadhi yao katika hospitali kuu ya mjini Beni na wengine katika vituo mbalimbali vya afya.

Ni watatu ndio hali yao inatajwa kuwa mahututi, kwa mjibu wa duru karibu na watabibu.

Vifo zaidi ya 3000 katika miaka mitano

Uchunguzi ukiwa unaendelea, ili kumkamata aliyelitega bomu hilo, msemaji wa jeshi la polisi mjini Beni amesema, kuwa watatangaza matokeo ya uchunguzi huo, ili raia waweze kujua kilichotokea.

Waasi wa Uganda wa ADF washukiwa

Tangu mwaka 2014, kundi la kigaidi kutoka Uganda ADF, limeshawauwa watu zaidi ya 3,000, katika mji na wilaya ya Beni mkoani Kivu ya Kaskazini na wilaya za Irumu na Mambasa katika mkoa jirani wa Ituri.

Na ili kuwatokomesha magaidi hao, majeshi ya Congo na Uganda, yamekuwa yakikabiliana nao katika eneo hili, yapata mwaka mmoja na miezi miwili sasa.

Chanzo: DW

Tarehe: 26.01.2023

Saa: 8 adhuhuri.

Tutumie maoni yako

 

Leave a Comment