Katibu mkuu mtendaji wa MCK, David Omwoyo. Picha/hisani

Nairobi, Kenya

Baraza la habari nchini Kenya (MCK) litakutana na wajumbe wa sekta ya habari kesho Ijumaa, Januari 27, 2023 kujadili mbinu mjarabu za kukabili wanahabari ghushi.

Katibu mkuu mtendaji wa baraza hilo David Omwoyo amesema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari mapema leo Alhamisi, kwamba mkutano huo umesukumwa na ongezeko la watu wanaojifanya wanahabari na kuishia kutapeli raia.

“Tumepata taarifa kwamba kuna wahuni wanajifanya wanahabari na kupenyeza kwenye hafla mbalimbali za kitaifa au kisiasa kwa nia ya kutapeli na kuhangaisha raia,” amesema Omwoyo.

“Kutokana na hili, Baraza la Habari la Kenya limeandaa mkutano na wadau Ijumaa hii, Januari 27, 2023, ili tujadili mbinu muafaka na mwelekeo wa kukabili suala hili kwa nia ya kuhimiza utaalamu na kukabili ongezeko la wanahabari hao feki.”

Katibu huyo, Omwoyo ameongeza kwamba baraza la MCK litahakikisha linaandaa mazingira mazuru ya wanahabari halisi kutendeakazi na kujaribu kuleta suluhu la changamoto zinazoikabli sekta hiyo.

“MCK itasalia msitari wa mbele kulinda maadili ya sekta ya habari na wanahabari ambao pekee wamepewa vitambulisho halisi na baraza hili kuhakikisha wanapewa nafasi ya kufanya kazi zao nchini Kenya kwa mujibu wa katiba ya nchi,” amesema.

Omwoyo amesisitiza kwamba baraza hilo linafanya kazi ndani ya mipaka yake kama inavyopambanuliwa kwenye sehemu ya 6(d) ya kanuni za baraza la Habari, ya mwaka 2013, inayoruhusu hamasa ya mabadiliko ya kitaaluma miongoni mwa wanahabari na vyombo vya habari.

Mwandishi: David Charo Ngumbao

Tarehe: 26.01.2023

Saa: 9 alasiri

Tuma maoni yako

 

Leave a Comment