Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, makamishna Boya Molu na Abdi Guliye. Picha/hisani

Nairobi, Kenya

Aliyekuwa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka  (IEBC) nchini Kenya, Wafula Chebukati anadai kupewa dau la rushwa kumtangaza kinara wa Azimio Raila Odinga kuwa mshinidi wa uchanguzi mkuu wa mwaka jana 2022 au uchaguzi urudiwe.

Mbele ya jopo linaoongozwa na wakili Aggrey Muchelule, leo Jumanne mchana, Chebukati amesema mnamo Agosti 15, mwaka 2022, watu watatu walimtembelea chumbani mwake alimokuwa amelala katika majengo ya Bomas, jijini Nairobi mwendo wa saa tisa alfajiri,na kumtaka aongee nao.

Hii leo ilikuwa muendelezo wa shuhuda za makamishna wa IEBC mbele ya jopo hilo la kuchunguza na kutathmini hali ilivyokuwa wakati wa uchanguzi mkuu wa mwaka jana 2022.

Jana Jumatatu, Abdi Guliye na mwenzake Boya Molu walitoa ushaidi mbele ya jopo hili linaloongozwa na wakili Agrey Muchelule.

Kwenye ushuhuda wake, Chebukati amesema watu hao watatu waliomtembelea ni aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju, seneta wa zamani wa Busia Amos Wako na wakili Kyalo Mbobu kujadili mustakabali wa matokeo ya uchanguzi.

“Nilipata taarifa kutoka kwa walinzi watu na wafanyakazi wengine wa IEBC kwamba kuna wanaume watatu wanataka kuniona. Waliingia bila kukaribishwa wakati nikiwa kwenye chumba cha mapumziko. Nilikuwa nimemwambia katibu mkuu mtendaji wangu kwamba nilihitaji kulala kwa saa moja hivi lakini niliamshwa na hawa watu watatu,” ameeleza Chebukati.

Mara baada ya kukaa, Chebukati anadai watatu hao walijitambulisha na kueleza sababu yao ya kumtembelea saa ile, ambayo ilikuwa kujadili zoezi zima la kujumuisha kura lilioendelea.

Anasema aliwaita upesi makamishna wote wa IEBC kabla ya kuendeleza mazungumzo yoyote na watu hao watatu.

“Walieleza lengo la kunitembelea kwamba walihitaji kuzungumze kuhusu zoezi la kujumuisha kura lililokuwa linaendelea na mimi nikawaambia ikiwa hilo ndo lengo ilikuwa lazima nihusishe makamishna wote tujadiliane,” amesema.

“Makamishna walikuwa karibu nailiwachukua dakika moja au mbili kujumuika nasi.”

Picha kubwa

Chebukati pia ameambia jopo hilo kwamba Amos Wako alikuwa wa kwanza kuzungumza akipendekeza kwamba tume hiyo ya IEBC ipinde baadhi ya kanuni ili ibailishe au ibatilishe matokeo ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa Chebukati, Tuju aliunga mkono pendekezo la Wako akisema ikiwa atakataa basi alazimishe marudio ya uchaguzi.

Kwenye ushuhuda wake uliorushwa mubashara na vituo mbalimbali vya runinga, Chebukati amesema watu hao walimuahidi zawadi kubwa endapo angetekeleza matakwa yao.

“Mzungumzaji wa kwanza alikuwa Amos Wako aliyesema hatupaswi kufanya kazi kwenye ombwe na lazima tutazame picha pana kwa ya taifa na kwamba katika hali kama hii unaweza kupindisha sheria kwa nia ya kuiokoa nchi,”amesema Chebukati.

“Tuju alisema ni muhimu sana tubadilishe matokeo kwa ajili ya Baba la sivyo taifa lingeelekea kwenye machafuko ya baada ya uchagzi. Nilielewa Baba kuwa Raila Odinga,” ameongeza Chebukati.

“Alisema afua nyingine ikiwa haiwezekani kubadilisha matokeo basi lazima tuhakikishe uchaguzi unarudiwa. Tuju alisema tukubali ofa hiyo kisha tutatuzwa. Hatukutaka apapambanue kuhusu tuzo hiyo.”

Mwenyekiti huyo wa zamani wa IEBC ameendelea kueleza kwamba aliweka mjadala huo wazi kwa makamishna wengine wachangie, ndipo Kamishna Irene Masit, akaunga mkono pendekezo hilo.

Lakini Chebukati anasema alikataa mtazamo wa Masiti akisisitiza kwamba wafuate kiapo cha kazi yao.

Haya yanakuja karibu miezi minne baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya.

Tangu juzi mgogoro mkubwa umeibuka kati ya serikali na upinzani huku viongozi wa pande zote mbili wakirushiana maneno makali.

Wadadisi wa mambo wanaonesha mgawanyiko juu ya chanzo cha mgogoro huu, wengine wakimkashifu Rais William Ruto kwa kutangaza kwenye vyombo vya habari kwamba kulikuwepo chama ya kuuawa kwa mwenyekiti wa IEBC na upinzani huku wengine wakimuunga mkono kwa kauli hiyo.

Inatumainiwa kuwa mgogoro huu utaisha haraka ili serikali iendelee kupambana na changamoto kubwa zinazolikumba taifa hili la Afrika Mashariki zikiwemo mfumko wa bei za bidhaa muhimu, baa la njaa na mabadiliko ya tabia nchini yanaoyoitikisha dunia.

Mwandishi: David Charo Ngumbao

Tarehe:  24.1.2023

Saa: 10 alasiri.

Tutumie maoni yako.

Leave a Comment