Mipira ya kondomu. Picha hisani

Taita Taveta, Kenya

Kaunti ya Taita Taveta inakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi, ARV na mipira ya kondomu karibu katika vituo vyote vya afya vya serikali na kibinafsi.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti uliofanywa na idara ya afya Kaunti hiyo juma lililopita, baada ya visa vya mimba za utotoni kuongezeka na kupindukia alfu 2000 Kaunti hiyo.

Tayari ongezeko kubwa la mimba za utotoni linashuhudiwa hasa maeneo ya mijini kama Voi inayoongoza kwa karibu visa 900 kulingana na waziri wa afya Kaunti hiyo John Mwakima.

Waziri Mwakima, ameambia wanahabari mara baada ya kuhudhuria mkutano juu ya ugonjwa wa Ukimwi katika ofisi ya vijana ya Voi kwamba serikali ya Kaunti hiyo ilianza kukumbwa na tatizo hilo mwanzoni mwa mwaka huu baada ya maambukizi ya virusi vya corona kuongezeka.

“Hali hii ilikuja mwanzoni mwa mwaka huu, tuna uhaba mkubwa wa mipira ya kondomu na dawa za ARV,” amesema Waziri Mwakima.

Shirika la kutetea haki za binadamu, Haki Africa lilizungumzia suala hilo miezi michache iliyopita lakini idara ya afya ikakana.

Kulingana na ofisa wa Haki Afrika Alex Mbela, wagonjwa wa Ukimwi walilazimika kugeukia vituo vya afya vya kibinafsi kupata ARV kwa gharama ya juu.

“Nilikuwa tayari nishaambiwa kwamba wagonjwa wa Ukimwi wanateseka na namjua mmoja ambaye alienda kituo cha afya cha kibinafsi kupata dawa za ARV lakini kwa gharama ya juu, Kaunti lazima ifanye jambo ,” amesema Alex.

Haya yanakuja wakati Kaunti hiyo ikiwa kwenye mgogoro mkubwa wa deni la shilingi milioni 60 za Kenya kati ya serikali ya Kaunti ya Taita Taveta na Mamlaka ya kusambaza dawa nchini Kenya (KEMSA) ambao umeathiri usambazaji wa dawa kwa miezi zaidi ya miezi 5.

Mwandishi: Fauzia Mohamed

Tarehe: 8.10.2021

Saa: 10 alasiri

Mrejesho: Tutumie maoni yako

Leave a Comment