
Mbu aina ya Anophelas anayesababisha Malaria. Picha/hisani
Kilifi, Kenya
Wanasayansi wanahofia madhara makubwa ya magonjwa yanayoonekana kusahaulika kutokana na juhudi kubwa kuelekezewa ugonjwa wa Covid-19 nchini Kenya.
Vyombo vya habari vinalaumiwa kwa kutoangazia magonjwa hayo yanayoua watu kimyakimya.
Emmaloise Gathuri, mmoja wa wanasayansi hao kutoka taasisi ya utafiti ya Kemri mjini Kilifi anasema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kusukuma uetekelezaji wa masuala yanayofungamana na afya kupitia uangaziaji.
Alipozungumza na mwandishi wa SBS Radio, Dickson Mwango Katana, Bi. Gathuri amesema tangu mripuko wa corona ulipotangazwa nchini, mwezi Machi mwaka jana 2020, maradhi kama Kifua kikuu, Malaria, Ukimwi, Kisukari na mengineyo ni kama yamesahaulika kwenye shajara za wanahabari.
Wanasayansi hao wanahofia kuwa huenda athari za maginjwa mengine zikaongezeka nchini Kenya kutokana na kushuka kwa juhudi za kuyaangazia.
Hii inatajwa kusababishwa na ugonjwa wa covid- 19 unaopewa kipaumbele zaidi na vyombo vya habari na asasi zingine za mawasiliano.
Tangu mripuko huo utangazwe Kenya, serikali imeelekeza juhudi kubwa kwa ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya corona.
Kwa sasa magonjwa kama malaria ulio tishio kubwa zaidi ya hata Covid-19 kulingana na shirika la Afya Ulimwenguni WHO, hasa barani Afrika hauangaziwi sana.
Emmaloise Gathuri ni mwanasayansi wa utafiti wa afya katika taasisi ya utafiti ya Kemri mjini Kilifi.
“Siwezi sema kwamba tumesahau magonjwa mengine tukaangazia magonjwa mengine, lakini kuna magonjwa mengi mengine ambayo labda vyombo vya habari havijaangazia sana, nan i hatari,” amesema Emmaloise.
Ugonjwa wa Covid-19 sio hoja ya kukosa kuangazia magonjwa mengine hatari kulingana na wanasayansi.
Mshirikishi wa muungano wa wanahabari Ukanda wa Pwani ya Kenya (KCA) Baya Kitsao ametoa wito kwa wanahabari kuangazia magonjwa mengine hatari mbali na corona, ili kuzuia madhara zaidi kwa jamii.
“Wanahabari kwa sasa wanaangazia sana ugonjwa wa Covid-19 hapa Kenya tangu ulipotangazwa. Kitu ninachowasihi wanahabari ni kwamba waangazie haya magonjwa megine kama Ukimwi, Kifua kikuu, Malaria ili nayo yasije yakachipuka kuwa hatari zaidi ya Covid-19,” ameambia SBS Radio.
Kulingana na takwimu kiasi cha watu milioni 10 huathirika na ugonjwa wa kifua kikuu kila mwaka kote duniani huku watu milioni 1.5 wakifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
Mataifa ya Afrika yanatajwa kuwa nyuma katika juhudi za kukabili magonjwa ya malaria na kifua kikuu.
Karibu asilimia 90 ya watu hufariki dunia kutokana na Malaria na kifua kikuu kila mwaka barani Afrika pekee huku ugonjwa wa ukimwi ukisalia tishio kwa afya ya binadamu kutokana na kukosa tiba.
Haya yanakuja wakati shirika la afya Ulimwenguni likiidhinisha chanjo ya kwanza ya Malaria aina ya RTS, S.
Mwandishi: Dickson Mwango Katana
Tarehe: 07.10.2021,
Saa: 7 mchana
Mrejesho: Tutumie maoni yako