
Samburu, Kenya
Wafugaji kutoka maeneo mbalimbali nchini Kenya wanatolea wito serikali inunue mifugo yao kama njia ya kuwasaidia kukabili hasara wanayopata kutokana na ukame.
Kaunti kama Samburu na Kilifi, jamii ya wafugaji inaitaka serikali iharakishe mpango wa kununua mifugo iliyoemewa na ukame.
Ng’ombe, Ngamia, Mbuzi na Kondoo katika Kaunti zilizoathirika na ukame wamedhoofika huku wanunuzi wakikosekana na wanaonunuliwa wakiuzwa kwa bei duni.
Wafugaji wanaofika katika masoko mbalimbali kuuza mifugo yao inawawia vigumu kufanikiwa, wakilazimika kuirejesha nyumbani kwa kuwa imedhoofika sana kiasi cha kutovutia wanunuzi.
Hivi sasa, wanaiomba serikali iharakishe mchakato wa kuwanunua kabla vifo zaidi havijatokea.
Wakazi wengi kutoka kaunti kame ikiwemo Kilifi wamekuwa wakishiriki ufugaji wa kuhamahama na mara nyingi hutegemea mifugo yao kwa mahitaji yao yote ya kimsingi.
Vifo vya mifugo hiyo kutokana na makali ya njaa iliyosababishwa na ukame, vimewaathiri mno.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame (NDMA), bei ya mifugo inaendelea kupungua kwa kasi ya kutisha huku ukosefu wa maji na lishe ukisababisha hali hiyo.
Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Abdul Bahari alisema Alhamisi wiki iliyopita kwamba watatafuta soko la mifugo hiyo kutoka Kiwanda cha Nyama (KMC).
Katika Kaunti Kilifi, serikali jana Jumanne ilianza kununua mifugo kutoka kwa wafugaji.
Kati ya bajeti ya Shilingi za Kenya milioni 450 iliyotengewa ununuzi wa mifugo kutoka Kaunti 10 zilizoathirika na ukame zaidi, Kaunti ya Kilifi imetengewa Shilingi milioni 9 zilizoanza kutumika kununua ng’ombe 450 kupitia kiwanda cha myama nchini KMC.
Kiasi cha Ng’ombe 170 na wengine 120 wanatarajiwa kununuliwa katika maneo bunge ya Ganze na Kaloleni yaliyoathirika zaidi na kiangazi pamoja na ukame.
Mwandishi: Mary Maria Karisa
Tarehe: 06.10.2021,
Saa: 11:30 jioni
Mrejesho: Tutumie maoni yako