
Beki wa Kariobangi Sharks FC Boniface Onyango akabiliwa na Kevin Kimani (Mwenye jezi nyeusi) wa Wazito FC wakati wa mechi ya Ligi kuu ya Kenya Ugani Moi International Sports Centre, Kasarani November 29, 2020. (Picha/Hisani)
Nairobi, Kenya
Beki kisiki wa klabu ya soka ya Kariobangi Sharks Boniface Onyango amethibitishwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Habari hizi zinakuja kama pigo kubwa kwa klabu hiyo yenye makazi yake eneo la Kariobangi nje kidogo ya jiji la Nairobi.
Mchezaji huyo aliumia neva za goti la mguu wake wa kushoto inayojulikana kitaalamu Patella tendinitis na kulingana na kocha wa mazoezi ya viungo John Kemboi atakaa nje kwa siku zisizopungua 28.
“Bonface Onyango ameumiza goti lake la kushoto vibaya. Amefanyiwa upasuaji na atakaa nje ya uwanja kwa kipindi cha karibu siku 28 hivi,” Kocha Kemboi amesema.
Mwezi Juni mwaka huu, Onyango aliumia eneo la paji lake la uso baada ya kugongwa wakati wa mazoezi, jeraha lililomfanya akose sehemu kubwa ya msimu wa 2020/2021.
Sharks wameratibiwa kucheza dhidi ya Bidco United ligi hiyo iliyosimamishwa itakaporejea wikendi ijayo.
Mwandishi: Samuel Kombe Karisa
Tarehe: 18.11.2021
Saa: 10 Alasiri