
Mwanariadha Agnes Tirop wakati wa moja wapo ya mashindano ya riadha. Picha/ hisani
Elgeyo Marakwet, Kenya
Mwanariadha wa mbio za mita 5,000 kwa wanawake na mwakilishi wa Kenya kwenye mashindano ya riadha ya Tokyo, Japan Agnes Tirop amekufa.
Bi. Tirop amekutwa leo Jumatano Oktoba 13 amekufa nyumbani kwake eneo la Iten, Kaunti ya Elgeyo Marakwet kusini mwa Bonde Ufa akiwa na majeraha ya silaha yenye ncha.
Polisi na wataalam wa alama za mwili wamefika eneo la tukio ila hawajatoa tamko lolote kuhusu kisa hicho cha kusikitisha.
Shirikisho la Wanariadha nchini Kenya (AK) kupitia rais walo Jackson Tuwei limeeleza mshangao mkubwa juu ya tukio hilo baada ya kuthibitishwa, likisema Kenya imepoteza ‘kito’ kwenye mchezo wa riadha.
“AK imesikitishwa sanana habari za kifo cha mshindi wetu wa nishani ya shaba kwenye mbio za dunia, mita 10,000 Agnes Tirop. Amekutikana ameuawa nyumbani kwake Iten, na inakisiwa ameuawa na mume wake. Tungali tunashughulika kufichua mengi zaidi kuhusu kifo chake,” amesema Tuwei.
“Kenya kwa kweli imepoteza kito muhimu sana kwa marehemu Agnes ambaye alikuwa mmoja wa wanariadha wanaokua kwa kasi mno katika ngazi za kimatifa kutokana na matokeo yake mazuri,” ameongeza kwenye taarifa yake.
Mwezi Septemba mwaka huu, Bi. Tirop alivunja rekodi ya wanawake ya mbio za kilomita 10 barabarani kwa kuandikisha muda wa 30:01 nchini Ujerumani.
Juma lililopita alimaliza wa pili kwa muda wa 30:20 kwenye mbio za Valencia Half Marathon.
Wasifu-kazi wa Bi. Tirop pia unajumuisha mbio za masafa marefu za dunia mwaka 2015 ambapo aliweka rekodi ya kuwa mwanariadha wa pili kinda kuwahi kushinda nishani kwenye ngazi ya dunia.
Alishinda pia mbio za masafa marefu Barani Afrika yaani Africa Cross Country Championship mwaka 2014 mjini Kampala, Uganda sanjari na mbio za vijana za dunia yaani World Junior Cross Country Championship mwaka 2013 mjini Bydgoszcz, Poland.
Mwandishi: Dickson Mwango Katana
Tarehe: 13.10.2021
Saa: 10 jioni.